Serikali ya kaunti ya Ksii imeimarisha matayarisho ya kukabiliana na athari za mvua ya El Niño inayotarajiwa kushuhudiwa nchini kuanzia mwezi ujao.
Hii ni kwa kuleta pamoja wakulima na wadau wa kilimo ili kuongeza uenezaji wa taarifa kuhusu tabia nchi.
Akizungumza wakati wa kongamano la maandalizi la siku mbili lililofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la FAO na kuandaliwa katika hoteli moja mjini Kisii, Afisa Mkuu wa Mifugo na Uvuvi wa kaunti hiyo Agnes Choti amesema ufasiri wa hali ya hewa umewadia kwa muda unaofaa.
Alielezea kuwa kaunti ya Kisii inatabiriwa kupokea maradufu ya kiwango cha kawaida cha mvua wakati wa kipindi kinachotarajiwa cha mvua ya El Niño.
Choti alidokeza kuwa wadau wanabaini maeneo yenye hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko na kusababisha madhara makubwa kwa mimea na mifugo ili waweze kuunda mpango wa hatua wa kaunti hiyo kwa lengo la kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.
Alitoa wito kwa serikali kutenga rasilimali za kutosha za kutekeleza mpango huo ili kuhakikisha usalama wa chakula na kulinda vyanzo vya mapato wakati wa mvua hiyo.
Taarifa ya Mercy Amoh wa KNA