Taasisi ya Mafunzo ya Tiba nchini Kenya, KMTC imeomba Bunge kukishinikiza serikali kujumuisha wanafunzi wake katika mpango wa mikopo na ufadhili wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, HELB.
Usimamizi wa taasisi hiyo unasema takriban wanafunzi 20,000 wanaopata fursa humo kila mwaka hukosa kuripoti kutokana na ukosefu wa fedha.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge, NG-CDF, inayoongozwa na Musa Sirma, Mkurugenzi Mkuu wa KMTC, Dkt. Kelly Oluoch, alisema wanafunzi 89,586 wa taasisi hiyo hawapati ufadhili wa serikali kwa sababu taasisi hiyo iko chini ya Wizara ya Afya badala ya Wizara ya Elimu.
Dkt. Oluoch alisema KMTC hufunza zaidi ya asilimia 85 ya wataalamu wa afya nchini Kenya, lakini wanafunzi wake hawana fursa ya kupata mikopo au ufadhili wa masomo kutoka kwa serikali, hali inayolazimu baadhi yao kuacha masomo.
Aliwataka wabunge kuhakikisha wanafunzi wa KMTC wanatambuliwa kama wanafunzi wa elimu ya baada ya sekondari wanaostahili kupata ufadhili sawa na wenzao katika taasisi nyingine.
Sirma alihoji sababu za KMTC kuachwa nje ya mpango wa ufadhili wa elimu wa Shilingi bilioni 300, huku Mbunge wa Kitutu Masaba, Clive Gisairo, akipendekeza KUCCPS iwajulishe waombaji mapema kuwa hakuna ufadhili wa serikali kwa kozi za KMTC.