Bodi ya utoaji wa mikopo ya kufadhili elimu ya juu nchini HELB, imetangaza uteuzi wa Geoffrey Monari, kama afisa mkuu mtendaji, wadhifa anaoshikilia rasmi kuanzia leo Machi 13, 2025.
Monari ana tajriba ya miaka 15 katika katika nyadhifa za juu za usimamizi wa masuala ya kifedha katika sekta ya elimu ya juu nchini.
Tangu mwaka 2020 hadi hivi punde, Monari amekuwa akihudumu kama afisa mkuu mtendaji wa hazina ya vyuo vikuu.
Kabla ya hapo, alihudumu kama afisa mkuu wa shughuli katika bodi ya kutoa mikopo ya elimu ya juu nchini HELB kati ya mwaka 2016 na 2020.
Katika kipindi hicho, alisimamia utekelezaji wa kimkakati wa mipango kadhaa ya mabadiliko kama vile kutoa mikopo kwa wanafunzi, kuboresha usimamizi wa madeni na kusaidia uhusiano kati ya HELB na washirika wake.
Monari ana shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara na shahada ya biashara. Anashikilia pia cheti cha mpango wa uongozi katika usimamizi wa kiwango cha juu.
Kwa sasa anasomea mpango wa elimu ya maafisa wakuu watendaji ulimwenguni katika chuo kikuu cha Strathmore.
HELB ina imani kwamba tajriba na ujuzi wa Monari vitatoa maono na uongozi unaohitajika katika kuinua bodi hiyo hadi viwango vipya ili kuhakikisha inaendelea kushughulikia wadau wake kwa ufanisi na uadilifu.