Mwanamuziki na mwanasiasa wa Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wije amemwomboleza kiongozi wa chama cha ODM nchini Kenya Raila Odinga ambaye aliaga dunia leo asubuhi.
Kiongozi huyo wa chama cha upinzani nchini Uganda NUP alifanya hivyo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii ambapo alichapisha picha zake za pamoja na Raila Odinga.
“Tumepokea habari za kifo cha Mheshimiwa Raila Odinga kwa huzuni kubwa. Alisimamia uhuru na heshima.” Aliandika Wine akiongeza kwamba tumepoteza kiongozi mkubwa wa Afrika ambaye alijitahidi kupigania watu hata ingawa alikutana na changamoto kadhaa.
Bobi Wine alimalizia taarifa yake fupi kwa kutoa ujumbe wa pole kwa watu wa taifa la Kenya na wapiganiaji wote wa uhuru kote ulimwenguni.
Wine alikuwa anamtambua Odinga kwa njia ya kipekee kwani alikuwa kiongozi wa upinzani kama yeye na huenda alijifunza mengi kutoka kwake.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliaga dunia leo asubuhi nchini India ambapo alikwenda kwa ajili ya matibabu.
Ujumbe unaoongozwa na waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi unatarajiwa kuelekea India leo kufanikisha usafirishaji wa mwili wa Odinga hadi humu nchini.
