Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi ataongoza ujumbe wa watu kadhaa watakaoelekea India kuurejesha humu nchini mwili wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Akitangaza rasmi kifo cha Raila wakati akihutubia taifa leo Jumatano alasiri, Rais William Ruto amesema ujumbe huo utaondoka nchini mara moja.
Ujumbe huo unajumuisha maafisa wa serikali na wanachama wa familia ya marehemu.
Upande wa familia utawakilishwa na mkewe Raila, Ida Odinga, Jaoko Oburu Odinga, Kevin Opiyo Oginga na wengineo.
Maafisa wa serikali watajumuisha Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Madini Hassan Joho, kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na kiongozi wa walio wachache Junet Mohamed.
Rais Ruto akidokeza kuwa serikali ya India, kufuatia ombi la Kenya, imeridhia kusaidia katika mipango ya kurejesha mwili wa marehemu Raila Odinga nchini.
Ruto pia amesema amesitisha shughuli zote za umma alizokuwa amepanga awali ili kutumia muda huo kuomboleza kifo cha kinara huyo wa ODM.
Amewataka maafisa wengine serikalini kufanya hivyo ili kutoa heshima kwa Raila katika kipindi cha siku saba zijazo za maombolezi.
“Tumempoteza mnara wa ujasiri, mnara wenye msimamo, na baba wa demokrasia. Hebu tuje pamoja, kama alivyotusihi daima, siyo kama wapinzani, lakini kama ndugu na dada waliounganishwa na mustakabali wa pamoja,” Ruto aliwasihi Wakenya wakati akihutubia taifa katika Ikulu ya Nairobi.
Aliandamana na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na kakaye Raila, Oburu Oginga, miongoni mwa viongozi wengine.
