Baadhi ya wawakilishi wadi wa kaunti ya Nairobi wa chama cha UDA na wanaomezea mate nyadhifa mbalimbali za kisiasa sasa wanataka mwelekeo.
Wanamtaka Rais William Ruto na uongozi wa chama hicho kuweka wazi mwelekeo wao wa kisiasa kufuatia hatua ya Gavana Johnson Sakaja kujiunga na chama cha ODM.
Kundi hilo, likiongozwa na mwakilishi mteule Cecilia Wairimu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya UDA, limesema chama kinapaswa kushughulikia mvutano unaozidi kujitokeza miongoni mwa wagombea wanaojiandaa kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Waliwalaumu viongozi wa juu wa UDA kwa kukaa kimya huku wenzao wa ODM wakiendelea kupokea wanachama wapya na kuimarisha ushawishi wao wa kisiasa.
Aidha, walitaka wagombea wote wa UDA waruhusiwe kufanya kampeni bila kuingiliwa na kupinga mipango yoyote ya kugawa maeneo ya kisiasa jijini Nairobi.
Wairimu alisema UDA itakuwa na wagombea wa ugavana, useneta, mwakilishi wa kike, ubunge na uwakilishi wadi, akisisitiza kuwa kuondoka kwa Sakaja hakutazuia juhudi za kukijenga chama katika maeneo bunge yote 17 ya Nairobi.
Alitaja hatua ya Sakaja kujiunga na ODM kuwa dharau kwa chama kilichomdhamini katika uchaguzi wa 2022 na kumuunga mkono wakati alipokabiliwa na jaribio la kung’olewa mamlakani.