Shirika la Msalaba Mwekundu, limesema takriban familia 300 zimeathiriwa na mafuriko katika kaunti ya Tana River.
Kupitia taarifa kwenye ukurasa wa X, shirika hilo limesema mto Wardesa ulivunja kingo zake na kuathiri familia hizo katika maeneo ya Eldera, Kono Ramadha na Mata Wardesa.
Kulingana na shirika hilo, barabara ya Kono Ramadha-Mlanjo, haitumiki kutokana na mafuriko hayo na kutatiza shughuli za uchukuzi.
“Maafisa wetu wanakadiria hali na wanashirikiana na utawala wa eneo hilo kuwaelekeza wakazi katika maeneo salama,” lilisema shirika la Msalaba Mwekundu.
Maeneo kadhaa nchini Kenya yanashuhudia mvua kupita kiasi na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.
Katika kaunti ya Kisumu, mvua iliyoandamana na upepo mkali ilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.