Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI imepanua huduma za uchakataji wa Cheti cha Kutokuwa na Rekodi ya Uhalifu almaarufu Police Clearance Certificate – PCC, kwa kutumia teknolojia ya kibiometriki katika kaunti za Turkana na West Pokot.
Upanuzi wa hivi karibuni wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Kibiometriki, MBIS umewezesha teknolojia hiyo kusakinishwa katika vituo vya Huduma Centre vya Lodwar na Kapenguria mtawalia, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mfumo huo unaotumia teknolojia ya kisasa ya kibiometriki umeleta mabadiliko makubwa katika uchakataji wa vyeti vya PCC kwa kupunguza muda wa kusubiri na kuongeza usahihi na ufanisi wa utambuzi wa wahalifu.
Huduma hiyo ambayo awali ilikuwa ikichukua angalau siku 14 za kazi sasa inaweza kukamilika kwa muda wa chini ya dakika tano.
Ili kuhakikisha mfumo huo unatumika ipasavyo, wafanyakazi wa Huduma Centre wamepatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu uendeshaji wake na namna ya kushughulikia maombi ya vyeti vya PCC.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuboresha huduma za usalama kupitia matumizi ya teknolojia bunifu, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Wakazi wa Turkana na West Pokot wamehimizwa kutembelea vituo vya Huduma Centre vya Lodwar na Kapenguria mtawalia ili kunufaika na huduma hizo zilizoboreshwa.