Mtaalamu na mshauri wa masuala ya vyombo vya habari nchini Uganda, Joel Isabirye, amepinga madai ya mwanamuziki Jose Chameleone kuhusu mradi uliokwana wa kituo cha runinga.
Chameleone alidai kwamba alipoteza shilingi milioni 250 pesa za Uganda katika mradi uliofeli wa kuanzisha kituo cha televisheni cha Leone Island TV.
Katika taarifa ya Novemba 10, 2026, Isabirye alikanusha kupokea kiasi hicho, akisema kwamba Chameleone alitumia jumla ya milioni 70 pekee katika hatua mbalimbali za mradi huo.
Katika mazungumzo ya moja kwa moja kwenye TikTok na mwanamuziki mwenza Bruno K, Chameleone alidai kwamba alimlipa mshauri ambaye hakumtaja jina, milioni 250 kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho, lakini akaishia kupata mawimbi ya majaribio badala ya kituo cha televisheni kinachofanya kazi.
Hata hivyo, Isabirye alipinga madai hayo, akieleza kuwa mradi huo haukukamilika kutokana na hatua ya Chameleone kutotimiza masharti ya leseni yaliyowekwa na Mamlaka ya Mawasiliano Uganda, UCC, kama vile kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha kuwa na mtaji wa kutosha.
Alisema fedha zilizotumika zilielekezwa katika kukodisha studio eneo la Makindye, kununua kompyuta za chumba cha udhibiti, kulipia ada za awali za leseni na kukodisha vifaa vya kupokea matangazo.
Chameleone awali pia alifichua kuwa gharama kubwa na changamoto za leseni zilimfanya kuachana na mipango ya kuanzisha kituo cha redio nchini Uganda, kabla ya kuanzisha kituo kingine nchini Burundi.