Mfanyakazi wa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), amefunguliwa mashtaka kwa madai ya kughushi cheti cha Chuo Kikuu, na kupokea shilingi milioni 8.5 kwa njia za ulaghai.
Betty Akinyi Odongo, anadaiwa alighushi cheti kutoka Chuo Kikuu cha Maseno, akisingiza kuwa ni halali aliyokabidhiwa baada ya kuhitimu na shahada ya utoaji ushauri nasaha.
Aidha, mshukiwa huyo anakabiliwa na mashtaka mengine ya kupata mali ya umma, kutengeneza stakabadhi bila idhini na kuwasilisha stakabadhi bandia.
Mahakama ilifahamishwa kuwa kati ya Oktoba 16, 2016 na Februari 5, 2024 akiwa katika halmashauri ya KRA Nairobi, Odongo anadaiwa kupata mali ya umma ya hadi shilingi 8,522,209.
Upande wa mashtaka uliongeza kuwa mshukiwa huyo aliteuliwa katika idara ya ukusanyaji ushuru wa ndani Jijini Nairobi tarehe 10 Oktoba, 2016.
Hata hivyo, Odongo alikanusha mashtaka hayo na aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja, pesa taslimu.