Takriban watu 17 wameuawa kwenye mashambulizi mawili tofauti ya risasi nchini Afrika Kusini.
Kulingana na ripoti ya polisi, wanaume wanane walipatikana wamefariki wakiwa na majeraha ya risasi katika eneo la Sweetwater, mjini Pietermaritzburg.
Saa kadhaa baadaye, watu wengine tisa walipatikana wamefariki katika eneo la Jeffsville, karibu na Jiji Kuu Pretoria, polisi wakisema miili hiyo ilikuwa na majeraha ya risasi.
Kamishna wa Taifa wa Polisi Fannie Masemola, amesema uchunguzi bado haujabainisha chanzo cha mauaji hayo.
“Mauaji haya hayakubaliki kamwe. Lazima tuwapate wahalifu hawa. Hatutawaruhusu wahalifu kuwahangaisha au kubainisha maisha ya wananchi,” alisema Masemola.
Kwa muda mrefu Afrika Kusini imeghubikwa na viwango vya juu ya uhalifu, huku mashambulizi ya risasi yakiongezeka na kusababisha maafa mengi.