Kenya na Tanzania zajadili mbinu za kuongeza mapato

Ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Tanzania uko nchini kwa ziara ya kujifunza na kubadilishana ujuzi kuhusu usimamizi wa fedha za umma.

Marion Bosire
2 Min Read

Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Bunge la Kitaifa la Kenya, ikiongozwa na Mwenyekiti Samuel Atandi, imepokea ujumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majirani hao wako nchini kwa ziara ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa fedha za umma.

Wabunge wa Kenya wamefanya mazungumzo na ujumbe huo wa Tanzania ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mashimba Mashauri Ndaki, kuhusu mbinu bora za kuchambua bajeti, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kukuza uwekezaji na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Atandi alisisitiza umuhimu wa Bunge kuwa na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa uangalifu na kuleta manufaa halisi kwa wananchi.

Alieleza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na ile ya kibinafsi ni njia muhimu ya kupata rasilimali za kugharamia miradi ya miundombinu na vipaumbele vingine vya maendeleo.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya fedha.

Atandi pia alielezea mfumo wa kikatiba wa Kenya unaosimamia matumizi ya fedha za umma, akibainisha kuwa uwazi, uwajibikaji, matumizi bora ya rasilimali na ushirikishwaji wa wananchi ni misingi muhimu katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti.

Mazungumzo hayo pia yalijikita katika nafasi ya vitengo vya kitaalamu vya Bunge katika kuwasaidia wabunge kuchambua mapendekezo ya bajeti, kufuatilia matumizi ya fedha na kuiwajibisha Serikali katika utekelezaji wa bajeti zilizoidhinishwa.

Ziara hiyo ya wiki moja inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mabunge hayo mawili na kuwezesha kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.

Share This Article