Huku taifa hili linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027, viongozi wa kisiasa wako mbioni kujiunga na vyama vya vikisiasa huku wengine wakibuni vyama vipya watakavyovitumia kuwania nyadhifa za kisiasa.
Wa hivi punde kubuni chama kipya cha kisiasa ni Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, aliyezindua chama cha Forum for Economic Development Agenda, FEDA, alichosema kitatetea usawa, haki na maslahi ya jamii zilizoachwa nyuma kimaendeleo.
Ole Lenku amebuni chama hicho baada ya kukigura chama cha ODM.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa chama hicho katika jumba la Ufungamano jijini Nairobi, Lenku alidokeza kuwa chama hicho kina sura ya kitaifa na kwamba ajenda yake itashughulikia pembe zote za taifa hili.
“Chama hiki ni cha kitaifa kwa sababu kitashinikiza usawa na haki kutoka ziwa Turkana Kaskazini mwa taifa hadi Taita Taveta Kusini mwa nchi,” alisema Gavana huyo.
Awali, Lenku alikuwa amedokeza kuwa alishauriana na wawakilishi wadi na wanaowania nyadhifa za kisiasa katika kaunti ya Kajiado na walikubaliana kubuni chama kipya cha kisiasa ambacho kitatumiwa na wawaniaji wote wa kisiasa katika maeneo yote ya jamii ya Maa, isipokuwa tu wadhifa wa Rais.