Mshukiwa anayedaiwa kumuua babake katika kaunti ya Baringo, amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.
Samuel Kibet Cherutich, aliyeshtakiwa kwa kumuua babake Reuben Chemwetich Cherutich, alipunguziwa mashtaka kutoka mauaji hadi kuua bila kukusudia.
Jaji wa Mahakama Kuu Mumbua T. Matheka, alitoa hukumu hiyo baada ya Kibet kukiri mashtaka hayo, kinyume na sehemu ya 202 ikiambatana na ile ya 205 ya sheria za nchi.
Mahakama ilifahamishwa kuwa mauaji hayo yalitekelezwa Septemba 5, 2020, saa nane mchana katika kijiji cha Turtur, kata ya Kabutie, kaunti ndogo ya Baringo Kaskazini.
Kulingana na mashahidi, Samuel alitekeleza mauaji hayo, baada ya babake kumuonya dhidi ya kufika shambani mwake.
Alipoghadhabika na onyo hilo, alichukua mshale na kumchoma babake kifuani na kusababisha kifo hicho.
Hata hivyo, Jaji huyo alisema licha ya kwamba mshtakiwa alisamehewa na familia yake, msamaha huo haukupunguza kiwango cha uhalifu huo.