LSK kuchunguza Wabunge Kaluma na Kaguchia

LSK ina wasiwasi kuhusu matamshi ya wanachama hao wawili na itatekeleza mchakato wake wa kinidhamu.

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha Wanasheria nchini, LSK kimeanzisha uchunguzi kuhusu matamshi yanayodaiwa kutolewa na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma na Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia, ambao ni wanachama wa LSK.

Katika taarifa, Rais wa LSK, Charles Kanjama alielezea kwamba semi za wawili hao zimesambazwa na kuripotiwa kwa wingi kuwa za uchochezi.

Alisema LSK ina wasiwasi kuhusu matamshi hayo na itatekeleza mchakato wake wa kinidhamu bila kujali hadhi ya kisiasa ya wabunge hao.

Kanjama aliipa Kamati ya Viwango vya Kitaaluma na Maadili ya LSK, kupitia Kamati Ndogo ya Maadili na Uhusiano wa Kinidhamu, agizo la kuchunguza rekodi zinazopatikana hadharani za matamshi hayo ndani ya siku 14 na kubaini iwapo yanakiuka maadili ya kitaaluma chini ya Kifungu cha 60(1) cha Sheria ya Mawakili.

Kulingana naye, kushikilia wadhifa wa kisiasa hakumsimamishi wakili kutekeleza wajibu wake wa kitaaluma na uhuru wa kujieleza kisiasa hauruhusu uchochezi wa ghasia au chuki.

Kanjama alifafanua kuwa uchunguzi au mashtaka yoyote ya jinai yatakayotokana na matamshi hayo yako chini ya mamlaka ya Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP na mahakama.

Iwapo ushahidi wa awali utabainika, kamati hiyo itawasilisha au kuwezesha kuwasilishwa kwa malalamiko rasmi dhidi ya mawakili hao wawili mbele ya Baraza la Nidhamu la Mawakili.

Kamati hiyo inapaswa kuwasilisha ripoti ya maendeleo kuhusu suala hilo kwa Baraza la LSK ndani ya siku 30.

Share This Article