LSK yataka kuanzishwa kwa fahirisi ya utawala wa sheria

Rais wa LSK Charles Kanjama, alisisitiza umuhimu wa kukabiliana na hali ya kutoadhibiwa kwa wanaokiuka sheria.

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha Wanasheria nchini Kenya, LSK, kimehimiza kuanzishwa kwa fahirisi ya utawala wa sheria ili kubaini mapungufu katika mfumo wa haki nchini na kuimarisha uwajibikaji.

Akizungumza katika mkutano wa wadau ulioandaliwa na Kamati ya Utawala wa Sheria ya chama, Rais wa LSK Charles Kanjama, alisisitiza umuhimu wa kukabiliana na hali ya kutoadhibiwa kwa wanaokiuka sheria, matumizi mabaya ya sheria na ukiukaji wa haki za kiraia na kisiasa.

Kanjama alisema fahirisi hiyo inayopendekezwa itasaidia kubaini maeneo yanayohitaji hatua za haraka na kuelekeza juhudi za kuimarisha uzingatiaji wa Katiba na upatikanaji wa haki.

Evans Ogada, mratibu wa Kamati ya Utawala wa Sheria ya LSK, alitoa changamoto kwa wadau kuhakikisha ahadi zilizowekwa katika Katiba zinatafsiriwa kuwa maboresho yenye manufaa katika maisha ya wananchi. Alisisitiza kuwa kila mtu lazima afuate sheria.

Kwa upande wake, Titus Kitonga kutoka shirika la Transparency International Kenya alihimiza kuanzishwa kwa mipango ya vitendo itakayonufaisha wananchi na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi.

Majadiliano hayo, yaliyoongozwa na Wanjiru Gikonyo mwanzilishi wa shirika la Visawe, yalilenga kuimarisha ushirikiano, kuendeleza elimu ya uraia na ushirikishaji, pamoja na kubaini hatua za kipaumbele zitakazotekelezwa katika kipindi cha miezi mitatu hadi kumi ijayo.

Kamati hiyo ilithibitisha kujitolea kwake kuendeleza ushirikiano, uratibu na uwajibikaji ili kuhakikisha misingi ya Katiba inaleta manufaa halisi kwa Wakenya.

Share This Article