Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Uganda, UPDF, limelalamikia kile ambacho linakitaja kuwa upendeleo wa wazi unaodhihirishwa na vyombo vya habari vya kimataifa kwa Bobi Wine.
Jeshi hilo limeishutumu vyombo hivyo vya habari vya Magharibi kwa kumpendelea Bobi Wine, kuwa rais ajaye wa Uganda, huku vikichapisha ripoti zinazolenga kumchafua mkuu wa jeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Katika taarifa iliyotolewa Oktoba 10, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Habari za Umma za Ulinzi, Kanali Chris Magezi, alipinga madai dhidi ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi katika makala ya Megan K. Stack yaliyochapishwa na gazeti la The New York Times.
Makala hayo yenye kichwa “The Authoritarian Future is Already Here” yalichapishwa Oktoba 8, 2026.
UPDF ilitaja madai yaliyomo kuwa yasiyo na msingi na kumshutumu mwandishi kwa kurudia maelezo yaliyotolewa na upinzani na wanaharakati.
“Kilicho wazi, hata hivyo, ni kwamba Jenerali Muhoozi Kainerugaba si mrithi anayependelewa na vyombo vya habari vya Magharibi katika Uganda ya baada ya Museveni,” alisema Magezi.
Aliongeza kusema kwamba wanahabari hao wangependelea Robert Kyagulanyi, “ambaye ni kibaraka wao”, awe madarakani, au watu wengine wenye misimamo inayofanana naye.
Magezi anahisi kwamba mustakabali wa Uganda ni chaguo ambalo litaamuliwa kikamilifu na Waganda wakati utakapofika.”
Magezi alitaja ripoti za awali zilizochapishwa na The Telegraph, The Wall Street Journal na The Economist kama mifano ya kile ambacho jeshi lilieleza kuwa “kampeni endelevu dhidi ya Kainerugaba”.