Wakenya wametakiwa kutohofu kwani serikali imeweka mikakati ya kutosha kukabiliana na visa vyovyote vinavyoweza kutokea vya ugonjwa wa Ebola nchini.
Hakikisho hilo linakuja siku chache baada ya Kenya kuthibitisha kisa kimoja cha ugonjwa huo.
Suala la ugonjwa huo limeangaziwa katika mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa na kuongozwa na Rais William Ruto.
Ni wakati wa mkutano huo ambapo Wakenya walihakikishwa kwamba hatua madhubuti za ufuatiliaji, ufanyaji vipimo na uangalizi tayari zimewekwa kukabiliana na ugonjwa huo.
Kwa upande mwingine, hospitali zimewekwa chonjo kushughulilikia visa vyovyote vinavyoweza kutokea vya ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya 4,000 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Wakati huohuo, jopokazi la kitaifa la kukabiliana na Ebola lilikutana leo Ijumaa ili kutathmini juhudi zilizopo za kukabiliana na kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo nchini Kenya.
Likiongozwa na Makatibu Dkt. Ouma Oluga wa Huduma za Matibabu na Mary Muthoni wa Afya ya Umma, jopokazi hilo liliafikiana kubuni makundi ya kushughulikia ufuatiliaji wa wanaokumbana na kutangamana na wagonjwa wa Ebola, kuboresha mawasiliano na kuchunguza visa vya ugonjwa huo.

Aidha, Wizara ya Afya itashirikiana na serikali za kaunti kutambua mapema visa vyovyote vya maambukizi ili kuzuia na kudhibiti maambukizi.