IEBC yaainisha masharti ya kuzingatiwa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Alhamisi wiki hii kujaza pengo lililoachwa na aliyekuwa mbunge wa hilo David Njuguna Kiaraho aliyefariki mapema mwaka huu.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon akiwahutubia wahabari Julai 14, 2026.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeainisha masharti mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa na wahusika wote hasa na wanasiasa na wapiga kura wakati wa uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ol Kalou. 

Uchaguzi huo ulioratibiwa kuandaliwa keshokutwa Alhamisi unatokana na kifo cha aliyekuwa mjumbe wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mapema mwaka huu.

Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ameonya kuwa wapiga kura hawataruhusiwa kupiga picha karatasi walizotumia kupigia kura na kisha kuzisambaza mitandaoni.

“Matumizi ya simu ya mkononi katika eneo la kupigia kura yamepigwa marufuku. Tungependa kuwakumbusha Wakenya na hasa wapiga kura wa Ol Kalou kwamba tafadhali usipige picha karatasi yako ya kupigia kura punde utakapomchagua mtu unayemtaka kuwa mbunge wako,” alishauri Ethekon wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumanne.

“Hii ni kwa sababu usufii na usiri wa kura unahitaji kuwa usimwambie yeyote uliyemchagua. Ikiwa utaweka hadhari karatasi ya kura, utashtakiwa na ukipatikana na hatia, utatozwa faini ya hadi shilingi milioni 1 na kufungwa kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu.”

Mwenyekiti huyo pia ametoa wito kwa wanasiasa na wafuasi wao kuepuka kujihusisha katika vitendo vinavyokiuka kanuni ya maadili ya IEBC ili kuruhusu kuandaliwa kwa uchaguzi huru, wa wazi na wa haki.

“Tunataka kuelezea bayana kuwa hatutaruhusu mtu yeyote, awe mwanasiasa mwandamizi au kiongozi katika nchi hii ambaye hajaidhinishwa na IEBC kuja na maafisa wao wa usalama au wafuasi kujaribu kuvuruga amani katika vituo vya kupigia kura,” alionya Ethekon.

Alikanusha madai ya kuhitilafiana na sajili ya wapiga kura akiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi wowote.

Maafisa zaidi ya 1,000 wa polisi wametumwa katika eneo bunge la Ol Kalou kuhakikisha usalama unadumishwa wakati wa zoezi la upigaji kura.

Eneo bunge hilo lina vituo 114 vya kupigia kura.

 

 

 

 

 

Share This Article