Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imetwaa ardhi ya umma ya thamani ya shilingi milioni 51 katika kaunti ya Mombasa.
Kulingana na EACC, ardhi hiyo MN/I/2411, yenye ukubwa wa ekari 0.514, inamilikiwa na Halmashauri ya Uchukuzi wa Angani nchini (KCAA).
Tume hiyo ilidokeza kuwa ardhi hiyo ilipatikana baada mzozo kuhusu umiliki wake kusuluhishwa kupitia njia mbadala za kutatua mizozo (ADR) mnamo Septemba 21, 2026, ambapo aliyekuwa amesajiliwa kama mmiliki wa ardhi hiyo Omar Tahir alikubali kuisalimisha kwa umma.
Uchunguzi wa EACC, ulbainisha kuwa ardhi hiyo ilikabidhiwa kwa njia haramu mwaka 2000 na aliyekuwa kamishna wa ardhi wakati huo Sammy Mwaita, kwa aliyekuwa mbunge wa Kuresoi Zakayo Kipkemboi Cheruiyot, ambaye baadaye alikabidhi ardhi hiyo kwa Omar Tahir.
Tume hiyo ilipongeza mfumo wa njia mbadala za kutatua mizozo, uliotamatisha miaka 17 ya kesi mahakamani, ikisema ardhi hiyo sasa ni ya umma na itatumiwa kuambatana na kusudi lake la awali.
Wakati huo huo, EACC imewahimiza wale wote wanamiliki ardhi ya umma kuikabidhi kwa hiari, ili kufanikisha ulinzi wa mali ya umma na kuepuka mchakato mrefu wa mahakama unaokumbwa na gharama za juu.