Botswana kuiga mfano wa Kenya kuboresha vyama vyake vya ushirika

Mwenyekiti wa chama cha akiba na mikopo cha huduma ya Taifa ya Polisi David Mategwa, alisema ziara hiyo iliashiria umuhimu wa taasisi za Afrika kujifunza kutoka kwa mbinu zilizofaulu ndani ya bara hili.

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya akutana Makamu wa Rais wa Botswana Ndaba Nkoisinathi Gaolathe.

Botswana inalenga kuimarisha sekta yake ya Vyama vya Ushirika, kwa kuiga mbinu bora za usimamizi wa sekta hiyo kutoka Kenya.

Makamu wa Rais wa Botswana Ndaba Nkosinathi Gaolathe ambaye anaongoza ujumbe wa ngazi  za juu kwenye ziara rasmi nchini Kenya, alitembelea Chama cha Akiba na Mikopo cha Huduma ya Taifa ya Polisi kujifahamisha na mbinu imara, endelevu na za kidijitali zinazotekelezwa katika sekta hiyo.

“Nidhamu ya wananchama wenu wa Bodi ya Usimamizi ni ya kupigiwa mfano. Tumejifunza mengi kutokana na utangamano wa leo. Tunafahamu kile ambacho tutaenda kutekeleza,” alisema Gaolathe wakati wa ziara hiyo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha Akiba na Mikopo cha Huduma ya Taifa ya Polisi David Mategwa, alisema ziara hiyo iliashiria umuhimu wa taasisi za Afrika kujifunza kutoka kwa mbinu zilizofaulu ndani ya bara hili.

“Tunaamini ujuzi kutoka hapa utafungua milango ya ushirikiano dhabiti kati ya taasisi zetu na kuchangia katika ukuaji wa vyma vya ushirika kote barani humu,” alisema Mategwa.

Ujumbe huo pia uliangazia jukumu pana la vyama vya ushirika katika kusaidia jamii kupitia elimu, huduma za afya, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya kijamii.

Share This Article