Bei za maziwa ni thabiti licha ya uhaba, yasema Bodi ya Maziwa ya Kenya

Martin Mwanje
1 Min Read

Bodi ya Maziwa ya Kenya (KDB) imehusisha uhaba wa maziwa unaoshuhudiwa katika baadhi ya maeneno nchini na hali za ukame na baridi zinazoshuhudiwa katika maeneo makuu ya uzalishaji wa bidhaa hiyo. 

Licha ya uhaba huo, KDB inasema bei ya maziwa kwa jumla inasalia thabiti, ingawa bei za bidhaa hiyo zimepanda katika baadhi ya maeneo.

Kwenye taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. William Maritim amehakikishia umma, watumiaji na wadau wa sekta ya maziwa kwamba bidhaa hiyo inaendelea kupatikana kwenye soko, licha ya changamoto za muda za usambazaji wake zinazoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo.

“Serikali inatekeleza hatua za kuimarisha uzalishaji wa maziwa na uthabiti wa mtungo wa usambazaji,” alisema Dkt. Maritim.

Hatua hizo zinajumuisha ununuaji na usambazaji wa vipozea vya maziwa ili kuboresha ukusanyaji wa maziwa na uhifadhi wake.

Kulingana na KDB, uwasilishaji maziwa kwa kampuni za uchakataji ulipungua kwa asilimia 3.7 kutoka lita milioni 84.4 mwezi Juni hadi lita milioni 81.3 mwezi Julai.

Share This Article