Mudavadi: Wakenya ughaibuni hutuma zaidi ya shilingi bilioni 700 nchini Kenya

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi akiwahutubia Wakenya wanaoishi Qatar.

Wakenya wanaoishi na kufanya kazi katika nchi za nje, hutuma nchini Kenya zaidi ya shilingi bilioni 700 kila mwaka. Hayo ni kulingana na Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.

Mudavadi alisema fedha hizo zimepiga jeki ukuaji wa uchumi hapa nchini na pia kubuni nafasi za ajira.

“Fedha hizo zimekuwa chanzo kikuu cha mapato ya kigeni na zimeshinda mapato yanayotokana na uuzaji wa Majani Chai, Kahawa, na Sekta ya Utalii zikijumuishwa pamoja,” alisema Mudavadi.

Akizungumza na raia wa Kenya wanaoishi na kufanya kazi nchini Qatar, Mudavadi aliyepia waziri wa Mambo ya Nje, aliwashauri kudumisha maadili na kuwa mabalozi wema wa Kenya wanapotekeleza majukumu yao.

“Nawahakikishia kujitolea kwa serikali kukabiliana na changamoto zilizosababishwa na kampuni bandia zinazotoa ajira ughaibuni, huku tukijizatiti kuona kuwa kila mkenya anayetafuta ajira nje ya nchi anahudumiwa kwa njia iliyo wazi na salama,” aliongeza Mudavadi.

Alisema serikali inashirikiana na mataifa kadhaa kuimarisha mikataba ya uhamiaji, ili kuhakikisha Wakenya wanapata kazi zilizo na malipo ya kumezewa mate kote duniani.

Website |  + posts
Share This Article