Bodi ya Utalii hapa nchini (KTB), imetangazwa bora zaidi barani Afrika, kwenye tuzo za Utalii za mwaka 2025 zilizoandaliwa Novemba 1,2025 Jijini London Uingereza.
KTB iliibuka mshindi baada ya kuzipiku bodi za Misri, Rwanda,Afrika Kusini na Cape Verde.
Wengine waliotajwa washindi ni pamoja na Mbuga ya Kitaifa ya Masai Mara, iliyotajwa kituo bora zaidi cha kitalii na hivyo kupiga jeki uongozi wa Kenya katika sekta ya kitalii barani Afrika.
Maasai Mara iliwapiga kumbo washindani wake Chobe, Kruger, Serengeti, South Luangwa na ile ya Volcanoes, kuibuka mshindi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Afisa Mkuu Mtendji wa KTB Allan Njoroge, alisema tuzo hizo ni ishara ya kujitolea kwa bodi hiyo kwa ukuaji endelevu wa Utalii hpa nchini.
“Tuzo hizi zinaashiria mikakati ya uvumbuzi iliyotekelezwa na KTB, ushirikiano na juhudi za pamoja za kuongeza idadi ya wageni wanaowasili, kuimarisha mapato na kubuni nafasi za ajira kwa wakenya,” alisema Njoroge.
Hafla hiyo iliandaliwa pembezoni mwa Mkutano wa Soko la dunia kuhusu Utalii wa mwaka 2025, Jijini Londona Uingereza.
