Idara ya Utabiri wa Hali ya hewa imetahadharisha kuhusu kutokea kwa mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo yenye milima magharibi mwa nchi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Katika taarifa, idara hiyo imesema kuna hatari ya radi katika Kaunti za Kisii, Kisumu na Narok, huku ikiwasihi wananchi kuepuka kujificha chini ya miti au kukaa karibu na madirisha yenye vifaa vya chuma wakati wa mvua kubwa.
Aidha, Idara hiyo imesema maeneo ya mijini yenye mifumo duni ya kupitisha maji, yako katika hatari ya kukumbwa na mafuriko ya ghafla na anawasihi wananchi kuepuka kutembea ama kuendesha gari kupitia maeneo yaliyofurika ili kuepuka kusombwa na maji.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa Edward Muriuki, amesema kwamba mvua ndogo katika eneo la mashariki mwa nchi inaweza kusababisha uhaba wa maji na malisho.Anaisihi jamii katika eneo hilo kuhifadhi maji na kutumia mbinu bora za matumizi ya maji.
Maeneo ambayo hayana mifumo ifaayo ya kupitisha maji na vichaka vinaweza kutoa mazingira mwafaka ya kuzaliana kwa mbu.
Muriuki anaonya kuwa ukosefu wa mifumo ya kupitisha maji inaweza kusababisha ongezeko la magonjwa yanayoenezwa na wadudu ikiwa ni pamoja na malaria na anatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuto za kiafya za kuzuia kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na wadudu.
