Wafanyakazi wa Posta kugoma kuanzia Oktoba 27

Dismas Otuke
1 Min Read
oplus_0

Wafanyakazi wa Shirika la Posta kote nchini wanatarajiwa kugoma kuanzia Jumatatu ijayo, Oktoba 27, endapo serikali haitawalipa malimbikizi ya mshahara wa miezi saba.

Chama cha Wafanyakazi wa Posta nchini, COWU, kilitangaza jana Jumatano kutoa makataa ya hadi Jumapili, Oktoba 26 kwa serikali kulipa malimbikizi ya tangu mwezi Aprili mwaka huu la sivyo wafanyakazi hao waanze mgomo wa kitaifa Oktoba 27.

Katibu Mkuu wa COWU Benson Okwaro amesema hali imekuwa ngumu kwa wafanyakazi hao kutoa huduma kwa kukosa kulipwa mshahara kwa kipindi cha miezi saba.

“Tumetoa makataa ya hadi Jumapili usiku kwa serikali kulipa mshahara wote wa miezi saba kufikia Jumapili la sivyo wafanyakazi wote watagoma kuanzia Jumatatu, Oktoba 27,” alionya Okwaro.

Aidha, wafanyakazi hao wanataka Shirika la Posta kuwasilisha shilingi bilioni 1.5 ambazo walikatwa kutoka kwa mishahara yao.

Shirika la Posta nchini lina wafanyakazi takriban 2,000.

Website |  + posts
Share This Article