Rais William Ruto ametetea serikali yake kwenye mpango unaoendelea wa kutoka hatimiliki katika eneo la Pwani, akisema serikali kamwe haitoi hatimiliki bandia.
Kwenye mahojiano na wanahabari mjini Mombasa Alhamisi usiku, kiongozi wa taifa alisema wale wanaotoa hatimiliki bandia ni matapeli na wakora, akidokeza kuwa serikali itakabiliana nao.
“Hatimiliki fake hazipatianwi na serikali, zinapeanwa na matapeli na wakora. Hizi ambazo tunazitoa sisi kama serikali tumezipima na tumezichunguza,” alisema Rais Ruto.
Aidha, alihakikisha kuwa wananchi walio kwenye ardhi ambapo kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kitajengwa katika kaunti ya Lamu, watafidiwa kikamilifu.
“Hakuna wananchi ambao tutawaondoa pale. Ardhi iliyoko pale ni ya serikali. Na kama kutakuwa na wananchi mahali kwingine ambapo tutatumia kuendesha kile kiwanda, serikali ya Kenya itawafidia,” alidokeza Rais Ruto.
Alitoa wito kwa wazee wa vijiji, viongozi wa dini,viongozi wa serikali na wale wa wakisiasa, kuhamasisha umma kujua umuhimu wa hatimiliki.