Katibu wa zamani wa Michezo Balozi Kirimi Kaberia ni miongoni mwa watu 6 walioshtakiwa kwa madai ya ubadhirifu wa shilingi milioni 330 za Mashindano ya Mataifa ya Afrika, CHAN.
Fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo mwaka 2018.
Wengine walioshtakiwa ni maafisa 3 wa zamani wa serikali na wakurugenzi wawili wa kampuni kwa madai ya kubadhiri kitita hicho cha fedha takriban miaka 8 iliyopita.
Kaberia alishtakiwa pamoja na Katibu wa zamani wa Michezo Stephen Njoroge Muthuma, Katibu wa zamani Mwandamizi wa Fedha katika Wizara ya Michezo Enock Ondwari Onditi na Mhasibu Mwandamizi wa zamani John Kiende Ruga.
Aidha, Mhandisi Mwandamizi wa zamani Samuel Mbaa Njoroge ambaye ni mkurugenzi katika kampuni za Taxwise Consulting Limited na Liroma Assurance Services Limited; na Anthony Mwangi Kimanthi, ambaye ni mkurugenzi katika kampuni ya Lease Pride Limited walifikishwa kizimbani kujibu mashtaka.
Walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Isabella Barasa wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani ili kujibu mashtaka.
Mashtaka dhidi yao nayo yaliidhinishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP aliyeridhika na uchunguzi uliofanywa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC.
Kesi hiyo inahusisha watuhumiwa 16, wakiwemo watu binafsi na kampuni, wanaokabiliwa na jumla ya mashtaka 17 yanayojumuisha utumizi mbaya wa mamlaka na kujipatia mali ya umma kinyume cha sheria.
Watuhumiwa 8 ambao ni Balozi. Kaberia, Stephen Njoroge Muthuma, Harun Chebet Komen, Enock Onditi Ondwari, John Kiende Ruga, Marcos Gonzales Puente, Auditel Kenya na Samuel Mbaa Njorog wanakabiliwa na mashtaka zaidi ya kukula njama ya kutekeleza uhalifu wa kiuchumi.
Upande wa mashtaka haukupinga kuachiliwa kwao kwa dhamana.
Hatua iliyoifanya mahakama kuwaachilia Balozi Kaberia kwa dhamana ya shilingi milioni 3 au milioni 1 pesa taslimu huku Stephen Njoroge, Enock Onditi, John Kiende, Anthony Mwangi na Lease Pride Limited, Samuel Mbaa Njoroge, Taxwise Consulting Limited na Liroma Assurance Services Limited wakiachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 2 au 600,000 pesa taslimu.
Kesi hiyo itatajwa Septemba 15, 2026.