Vijana wa hapa nchini wametakiwa kutumia vyema fursa za ajira zinazotolewa na serikali pamoja na mashirika mengine, ili kuimarisha maisha yao.
Kiongozi wa nchi alidokeza kuwa serikali imeweka mikakati dhabiti kubuni nafasi za ajira kwa vijana ikiwa ni pamoja na katika viwanda kama kile kinachojengwa cha kusafisha mafuta cha Dangote kaunti ya Lamu.
“Mimi nataka vijana wa Kenya kila mmoja wao ajitume. Leo nimesimama pale Likoni nimewaambia vijana wa Mombasa, pale Lamu kuna nafasi za ajira 60,000. Vijana wa Mombasa wakijipanga wajitume, nafasi kama 5,000 za ajira zitapatikana pale Lamu,” alisema Rais Ruto.
Kwenye mahojiano ya moja kwa moja na wanahabari mjini Mombasa Alhamisi usiku, Rais Ruto alitaja baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa na serikali katika eneo la pwani ambayo imetoa fursa tele za ajira kwa vijana.
“Hapa Dongo Kundu tunamalizia kutakuwa na nafasi za ajira pale, hapa Mombasa tunajega nyumba za gharama nafuu 12,000, ujenzi wa nyumba 2,200 zimeanza Changamwe, tunahitaji vijana 1,000 likoni,” alisema Rais Ruto.
Wakati huo huo, alidokeza kuwa katika muda wa miaka minne iliyopita vijana 680,000 wa Kenya walipata ajira ughaibuni, huku akiwahimiza vijana kutumia Halmashauri ya kitaifa ya Ajira kupata kazi katika mataifa ya ng’ambo.