Serikali iko mbioni kuboresha uratibu, ufadhili na ushirikishaji wa umma katika mpango wake wa mawasiliano chini ya Sera ya Mawasiliano ya Serikali Kuu.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Idara ya Utangazaji Stephen Isaboke.
Sera hiyo inaunganisha mawasiliano serikalini, kuanzisha chanzo kimoja cha ukweli na kubainisha majukumu ya maafisa na miundo ya mawasiliano.
Akizungumza wakati wa mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini leo Jumanne, Isaboke alilalama kuwa yamkini hakujakuwa na mawasiliano madhubuti juu ya maendeleo na mageuzi yanayofanywa serikalini huku mipango ikikosa kuangaziwa ipasavyo.
Mfumo mpya unayachukulia mawasiliano kama kiungo muhimu cha maendeleo na wala siyo shughuli inayoanzishwa muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa miradi.
“Tunakiri kwamba mawasiliano ndio mhimili mkuu wa serikali yoyote; hivyo, mawasiliano yanapaswa kupewa kipaumbele kuanzia mwanzo. Katika sera mpya, miradi itajumuisha kipengele cha mawasiliano na rasilimali za kuieleza kwa umma, na mambo yote ambayo yatapimwa kwenye mizani,” alisema Isaboke.
Kulingana na Katibu huyo, mawasiliano sasa yatakuwa sehemu ya utendaji kazi huku wizara zikitakiwa kutekeleza miradi na kutoa maelezo juu yake kwa umma.
“Siyo tu kwamba: Tumetekeleza mradi huo? Pia ni: Tumetoa mawasiliano ya kutosha kuuhusu?” aliongeza Isaboke.
Mpango wa mawasiliano wa serikali unahusisha maafisa wa mawasiliano wa Rais na Urais, Naibu Rais, Mawaziri, Makatibu, Msemaji wa Serikali, Maafisa wa Mawasiliano wa Wizara, mifumo ya kaunti na Maafisa wa Utawala wa Serikali Kuu wakiwemo Machifu na Manaibu wao.
Katibu Isaboke ameuelezea mpango huo kama okestra, huku wahusika mbalimbali wakitekeleza majukumu tofauti kuelekea lengo moja.