Uhuru ampa Matiang’i mikoba ya uongozi wa Jubilee

Uteuzi wake unatarajiwa kuidhinishwa katika Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe, NDC.

Marion Bosire
1 Min Read

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amempa Dkt. Fred Matiang’i mikoba ya uongozi ya chama cha Jubilee, JP.

Dkt. Matiang’i, ambaye amekuwa akihudumu kama Naibu Kiongozi wa JP, atashikilia wadhifa huo akisubiri uteuzi wake kuidhinishwa katika Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe, NDC.

Katika mkutano wa viongozi wa chama hicho leo, Uhuru alitangaza kwamba atasalia kuwa mwanachama wa JP huku pia akitoa huduma kama mshauri mkuu wa chama.

Dkt. Matiang’i katika hotuba yake ya kukubali uongozi wa chama, aliahidi kuendeleza uongozi mwema wa chama kutoka mahali ambapo Rais mstaafu ameachia.

“Ulivyoniamini, ninataka nikuhakikishie kwamba sitakukatisha tamaa,” aliahidi Waziri huyo wa zamani wa Usalama wa Taifa.

Mnamo Septemba 3, 2026, Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilidumisha sheria inayowazuia Marais wastaafu kushikilia nyadhifa za uongozi katika vyama kwa muda unaozidi miezi 6 baada ya kustaafu.

Afisi ya Rais wa 4 wa Jamhuri ya Kenya, ilielezea kwamba kucheleweshwa kwa mchakato wa kuachia uongozi wa chama cha Jubilee kulisababishwa na mgogoro wa ndani.

Mgogoro husika ulihitaji ufafanuzi wa kisheria.

Share This Article