SDA yasherehekea mamlaka ya muda ya kuendesha Chuo Kikuu cha Kamagambo

Rais William Ruto alikabidhi Chuo Kikuu cha Waadventista cha Kamagambo Barua ya Mamlaka ya Muda, katika ikulu ndogo ya Kisumu.

Marion Bosire
2 Min Read

Kanisa la Waandventista wa Sabato, SDA nchini Kenya na hasa West Kenya Union Conference, linasherehekea mamlaka ya muda ambayo lilikabidhiwa ili kuendesha chuo kikuu.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kukipa Chuo Kikuu cha Waadventista cha Kamagambo Barua ya Mamlaka ya Muda, katika ikulu ndogo ya Kisumu.

Kanisa hilo limeelezea hatua hiyo kuwa kilele cha miaka ya maombi, maono, bidii na uvumilivu kutoka kwa wadau mbalimbali waliohusika katika safari ya chuo hicho.

Katika ujumbe uliotolewa kwenye mitandao ya kijamii, Muungano wa West Kenya ulisema mafanikio hayo ni zaidi ya sherehe, ukieleza kuwa ni hatua iliyosubiriwa kwa muda mrefu na taasisi hiyo pamoja na jamii pana ya Waadventista.

Muungano huo uliwapongeza viongozi wa chuo, wafanyakazi na wanafunzi, pamoja na waumini wa kanisa na wengine waliochangia katika maendeleo ya taasisi hiyo.

Kutolewa kwa Barua ya Mamlaka ya Muda kunafungua ukurasa mpya kwa Chuo Kikuu cha Waadventista cha Kamagambo, huku kikiendelea na shughuli zake na maendeleo yake kama taasisi ya elimu ya juu.

Kanisa hilo limeeleza matumaini kuhusu mustakabali wa chuo hicho, likisema hatua hiyo inastahili kusherehekewa huku likisisitiza kuwa safari ya maendeleo bado inaendelea.

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha nafasi ya taasisi hiyo katika kuendeleza dhamira ya Kanisa la Waadventista katika elimu na kutoa fursa za elimu ya juu.

Muungano wa West Kenya ulimalizia ujumbe wake kwa kukipongeza Chuo Kikuu cha Waadventista cha Kamagambo na kueleza imani yake kuhusu mustakabali wa taasisi hiyo.

Share This Article