Mwigizaji maarufu nchini Tanzania, Kajala Frida Masanja ameamua kutumia njia za kisheria kumkomesha mkosoaji wake mkuu Mwijaku.
Kupitia kwa mawakili wake, Kajala amemtaka Burton Mwemba maarufu kama Mwijaku kuacha mara moja kutoa, kuchapisha au kusambaza kauli wanazodai zinamdhalilisha na kumchafulia jina.
Katika barua ya kisheria iliyotumwa kwa Mwijaku, mawakili hao wamedai kuwa video na kauli zake zinazomhusu Kajala zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii na zinaweza kuharibu heshima, sifa na maslahi yake ya kibiashara.
Mawakili hao wamemtaka Mwijaku aondoe video, machapisho na maudhui yote yanayolalamikiwa, pamoja na kutoa ahadi kwa maandishi ndani ya saa 48 kwamba hatarudia kufanya hivyo.
Aidha, Kajala kupitia mawakili wake amemtaka Mwijaku kulipa fidia ya shilingi milioni 200 pesa za Tanzania, ndani ya siku 14 kama fidia kwa madai ya madhara ya sifa, msongo wa kihisia, madhara ya kijamii pamoja na hasara za kiuchumi na kibiashara.
Barua hiyo imeongeza kuwa endapo Mwijaku hatatekeleza matakwa hayo ndani ya muda uliowekwa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila kupatiwa taarifa nyingine.