Uhuru aridhia uamuzi wa mahakama kuhusu uongozi wa Jubilee

Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi, aliamua kwamba marais wastaafu wamezuiwa kisheria kushikilia uongozi wa chama kwa zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka madarakani

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amekaribisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha Kifungu cha 6 cha Sheria kuhusu Mafao ya Kustaafu kwa Marais.

kulingana naye, uamuzi huo unathibitisha ukomavu wa kidemokrasia wa Kenya na heshima kwa mahakama.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Septemba 15, 2026, kupitia ofisi yake, Uhuru alisema uamuzi wa Jaji Lawrence Mugambi haupaswi kuchukuliwa kama kizuizi kwa maisha yake ya kisiasa, bali kama uthibitisho wa kuheshimu utawala wa sheria.

Rais huyo wa zamani pia alizungumzia kuchelewa kwa makabidhiano ya uenyekiti wa Chama cha Jubilee, akisema mchakato huo ulikwama kutokana na mzozo wa ndani uliokuwa ukihitaji ufafanuzi wa kisheria, na wala si kwa sababu ya kusita.

“Kwa mwongozo wa mahakama, njia hiyo sasa iko wazi,” taarifa hiyo ilisema.

Uhuru alithibitisha utayari wake wa kuhakikisha makabidhiano ya uongozi yanakamilishwa kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria na katiba ya Chama cha Jubilee.

Alisema anatarajia shughuli za chama kuendelea bila vikwazo.

Aidha, Uhuru alisema anakaribisha ukurasa mpya wa Jubilee unaozingatia katiba ya chama, utawala wa sheria na kizazi kijacho cha viongozi.

Jana Septemba 14, 2026, Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi alitupilia mbali ombi lililokuwa likipinga lililopinga Kifungu cha 6 cha Sheria ya Manufaa ya Kustaafu kwa Rais.

Aliamua kwamba marais wastaafu wamezuiwa kisheria kushikilia nyadhifa za uongozi katika chama chochote cha kisiasa kwa zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka madarakani.

Share This Article