Washukiwa wa wizi duka la M-Pesa Yatta wakamatwa

Martin Mwanje
1 Min Read

Washukiwa watatu wanaohusishwa na wizi wa shilingi 169,000 kwenye duka la M-Pesa katika eneo la Katangi, kaunti ndogo ya Yatta wamekamatwa.

Mhudumu wa duka hilo aliibiwa fedha hizo Mei 15, 2026 na wezi hao kwenda mafichoni.

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema watatu hao walikamatwa wakati wa operesheni ya polisi iliyoratibiwa kwa uangalifu mkubwa.

Wakiifanya operesheni hiyo baada ya kupokea vidokezo kutoka kwa umma, maafisa kutoka eneo la Katangi walichukua hatua za haraka na kumkamata mmoja wa washukiwa, Ben Mutuku, katika soko la Katangi.

Kisha msako wao ulisababisha kukamatwa kwa washukiwa wengine wawili,  Simon Makau na Samuel Mbolu, katika eneo la Yathui katika kaunti ndogo ya Mwala.

Wawili hao walikamatwa wakati wakisafiri kwenye gari jeupe aina ya Toyota Corolla, nambari za usajili KDU 164G.

Wakati wa operesheni hiyo, simu ya M-Pesa iliyotumiwa kwenye duka hilo na ilikuwa imeibwa pia ilipatikana.

Washukiwa wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article