Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye, amelazwa katika hospitali ya JCRC baada ya afya yake kuzidi kudhoofika gerezani Luzira.
Mkewe Besigye aitwaye Winnie Byanyima, alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X kwamba mumewe alihamishwa kwenda hospitalini baada ya giza kuingia siku ya Ijumaa.
Alimtaja kuwa “dhaifu sana,” akisema anapata shida kutembea, kuzungumza, kuandika na hata kushika vitu kwa uthabiti.
Byanyima amerejelea ombi lake kwa mamlaka kumruhusu kumpeleka Besigye Geneva, nchini Uswisi, kwa ajili ya matibabu maalumu na kupata huduma ya afya akiwa karibu na familia yake.
“Anahitaji huduma, si ukatili,” Byanyima alisema, akisisitiza kuwa Besigye hapaswi kuhamishwa kutoka eneo moja hadi jingine akiwa katika hali mbaya ya kiafya.
Besigye amekuwa kizuizini tangu Novemba 2024 huku akiendelea kukabiliwa na kesi zinazohusiana na masuala ya usalama na uhaini.
Chama chake cha People’s Front for Freedom (PFF) pia kimeeleza wasiwasi kuhusu hali yake na kutaka madaktari wake binafsi waruhusiwe kumfikia bila vikwazo.
Uhamisho huo wa hivi karibuni umeongeza wasiwasi kuhusu afya ya mwanasiasa huyo mkongwe wa upinzani, ambaye amekuwa kizuizini kwa miezi kadhaa huku mapambano yake ya kisheria yakiendelea.