Swangz Avenue yafafanua kuondoka kwa Zafaran

Mmoja wa waanzilishi wa kampuni hiyo Benon Mugumbya amekanusha madai ya ugomvi.

Marion Bosire
2 Min Read

Kampuni ya burudani ya Swangz Avenue ambayo inajihusisha na usimamizi wa wasanii imefafanua kuhusu hatua ya Zafaran ya kuondoka kwenye kampuni hiyo.

Mmoja wa waanzilishi wa kampuni hiyo Benon Mugumbya amekanusha madai ya utata kugubika mchakato huo akisema waliafikiana kiungwana na kwamba hatua hiyo ilichochewa na biashara.

Baada ya Zafaran kutangaza rasmi kwamba ameondoka Swangz, maswali yalijiri huku wengi wakikisia kwamba kulikuwa na matatizo.

Hata hivyo msanii huyo hakutoa maelezo ya sababu za kuondoka ila alielezea kwamba amebadili jina la kisanii na kuzindua jukwaa jipya kwenye YouTube.

Benon alielezea kwamba pande zote mbili ziliafikia makubaliano ya kusitisha ushirikiano baada ya kutathmini uhusiano wa kibiashara na kuhitimisha kwamba hakukuwa na faida.

Kingine alichokifafanua Benon ni kwamba walichelewa kutangaza hatua hiyo kwa sababu Zafaran alikuwa bado chini ya masharti fulani ya mkataba.

Sababu nyingine ni kwamba Zafaran aliomba muda kabla ya kufichuliwa kwa habari hizo kwa umma.

Uvumi kuhusu kuondoka kwa msanii huyo kwenye kampuni hiyo ilisheheni mitandao ya kijamii mwezi Februari mwaka huu wa 2026 lakini baadaye ukafifia hadi wakati alipotangaza rasmi mwezi uliopita.

Benon anasema kampuni ilishtukia tu kwamba Zafaran ametangaza kuondoka kwake bila kuijuza lakini akasisitiza kwamba hakuna ugomvi kati ya kampuni na msanii huyo.

Katika taarifa yake, Zafaran ambaye sasa amebadili jina hadi Zafar aliishukuru kampuni ya Swangz kwa aliyoafikia.

Share This Article