Argentina yanusurika kutafunwa na Papa wa Cape Verde

Licha ya kubanduliwa, Cape Verde wameaga Kombe la Dunia bila kupoteza mechi ndani ya dakika 90, wakitoka sare mara nne.

Dismas Otuke
1 Min Read

Limbukeni Blue sharks kutoka Cape Verde walitoka nyuma mara mbili na kuwashika mateka mabingwa wa Dunia Argentina katika sare ya bao 1, kabla ya kubanduliwa 3-2 katika muda wa ziada wa mechi ya raundi ya 32 ya Kombe la Dunia mapema Jumamosi uwanjani Miami.

Nahodha Lionel Messi aliweka mabingwa watetezi uongozini kwa bao la dakika ya 29 kabla ya Deroy Duarte kuwarejesha mchezoni Cape Verde kunako dakika ya 59 na mechi kumalizikia sare ya 1-1.

Katika dakika 93, Lissandro Martinez alitikisa wavu lakini Sidny Lopez akasawazisha dakika 103 na kufanya mambo kuwa 2-2.

Mechi ikikaribia kumalizika, Diney Borges alijifunga bao kwa kichwa na kuwazawadi Argentina ushindi na sasa watachuana na Misri katika raundi ya 16.

Licha ya kubanduliwa, Cape Verde wameaga Kombe la Dunia bila kupoteza mechi ndani ya dakika 90, wakitoka sare mara nne.

Share This Article