Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ameelezea umuhimu wa mfumo wa elimu nchini kuwapa vijana ujuzi, maarifa na imani ili kuwawezesha kushindana mahali popote duniani.
Ili kufikia hilo, amesema mageuzi mbalimbali kwa sasa yamewasilishwa bungeni kwa lengo la kuuboresha mfumo huo.
“Ili kuhakikisha mageuzi haya ni sahihi inahitaji Serikali, Vyuo Vikuu, taasisi za kidini na washikadau wengine kusemezana mezani,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
“Siku za baadaye tunazotazamia za Kenya zinaanza na namna tunavyoandaa kizazi kitakachoijenga.”
Kadhalika, Mudavadi alikariri umuhimu wa kuwaandaa vijana nchini siyo tu kwa ajira za leo bali pia za hiyo kesho, akielezea umuhimu wa taasisi za kidini katika kufikia azimio hilo.
Aliyasema hayo alipokutana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Tangaza kuzungumzia namna ya kushirikiana katika kufanikisha mageuzi yaliyopendekezwa kufanyiwa mfumo wa elimu nchini.