2 wafariki, 6 wajeruhiwa kwenye ajali eneo la Taru

Ajali hiyo iliyohusisha basi na trela ilitokea eneo la Taru kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi leo Jumatano asubuhi. 

Martin Mwanje
1 Min Read

Watu wawili wameripotiwa kufariki kwenye ajali ya barabarani iliyohusisha basi la Dreamline lililokuwa na abiria 52 na trela. 

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Taru kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi leo Jumatano asubuhi.

Afisa wa trafiki wa kanda ya Pwani Asha Wario anasema ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo kugonga trela iliyokuwa imesimama.

Mtu mmoja alifariki papo hapo huku mwingine akiaga dunia alipokuwa akikimbizwa hospitalini.

Kwa upande mwingine, watu 6 walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa Coast General Hospital kwa matibabu.

Wario akimnyoshea lawama dereva wa trela kwa kukosa kuweka alama za kuwatahadharia madereva wengine juu ya kusimama kwa trela hiyo.

Afisa huyo ametoa wito kwa madereva kwenye barabara hiyo kuwa waangalifu hasa wakati wa asubuhi akielezea kuwa ajali nyingi hutokea majira hayo.

 

 

 

 

 

Share This Article