Malindi yatakiwa kuimarisha miundombinu kabla ya El Nino

Kamati ya Bunge la Senate kuhusu Ugatuzi na Uhusiano baina ya Serikali, ilisema hatua hiyo inalenga kukabiliana na hatari ya kuzuka kwa magonjwa kama vile kipindupindu.

Tom Mathinji
2 Min Read
Mohamed Abbas - Seneta wa kaunti ya Wajir.

Maafisa wa manispaa ya Malindi, wameagizwa kuhakikisha miundombinu inaimarishwa kabla ya kuanza kwa mvua za El Nino, zinazotarajiwa kuanza mwezo Oktoba.

Kamati ya Bunge la Senate kuhusu Ugatuzi na Uhusiano baina ya Serikali, ilisema hatua hiyo inalenga kukabiliana na hatari ya kuzuka kwa magonjwa kama vile kipindupindu na majanga mengine ya afya ya umma.

Agizo hilo lilitolewa wakati kamati hiyo ilipokutana na bodi ya usimamizi wa Manispaa ya Malindi Alhamisi asubuhi, kwenye mpango wa Senate Mashinani kaunti ya Kilifi.

Maseneta hao wakiongozwa na mwenyekiti Mohamed Abbas ambaye ni Seneta wa kaunti ya Wajir, walielezea kutamaushwa kwao kutokana na utoaji wa kile walichotaja kuwa huduma duni kwa wakazi wa eneo hilo.

Mwanachama wa kamati hiyo Margaret Kamar, ambaye ni Seneta maalum, alidokeza kuwa huduma zinazotolewa na manispaa ya Malindi haziafikii viwango vya huduma katika maeneo ya mijini.

“Manispaa haiwezi kuwa manispaa, ikiwa haina mfumo wa bomba la kupitishia majitaka,” alisema Kamar.

Hata hivyo, kwa upande wake, bodi ya usimamizi wa manispaa ya Malindi ikiongozwa na mwenyekiti Suleiman Salim Omar, ilielezea kuwa fedha za kutosha zimetengwa kukabiliana na mafuriko endapo yatatokea.

“Tumesimamisha baadhi ya miradi ya maendeleo, katika juhudi zetu za kukabiliana na athari za mvua ya El Nino,” alisema Omar.

Aidha, meneja wa manispaa hiyo Furaha Chome, alisema kati ya wafanyakazi 276, wengi wao wanatekeleza jukumu la kusafisha mitaa na mitaro ya kupitisha maji ili kudumisha usafi wa kimsingi.

Bunge la Senate limekuwa likiandaa vikao vyake katika kaunti ya Kilifi, kwenye mpango wake wa kila mwaka wa Senate Mashinani.

Share This Article