Serikali ya Kenya Kwanza haijayumba katika kufanyia kazi manifesto yake inayolenga kutekeleza miradi ya maendeleo kila sehemu ya nchi.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema hadi kufikia sasa, kaunti zote 47 zimenufaika na miradi mikubwa ya maendeleo kama ilivyoahidiwa katika manifesto ya Kenya Kwanza huku miradi mingine zaidi ikipangwa kutekelezwa.
“Tunatekeleza manifesto ya UDA hatua kwa hatua, ukurasa kwa ukurasa, sura kwa sura. Sina shaka tutaitekeleza kikamilifu,” alisema Prof. Kindiki.
“Nafuatilia utekelezaji wa manifesto hiyo kila siku, ukurasa kwa ukurasa, kwa sababu nafahamu kilichomo. Ni mimi niliyeiandika.”
Naibu Rais aliyasema hayo leo Jumatano asubuhi alipokagua miradi ya maendeleo katika eneo bunge la Maragua, kaunti ya Murang’a.

Alikagua ujenzi wa uwanja wa Gakoigo unaojengwa kwa kima cha shilingi milioni 900 na uwekaji lami kwenye barabara ya Kigoro-Matanya-Mung’etho-Muchagara-Kiambaa yenye urefu wa kilomita 16 kwa unaofanywa kwa kima cha shilingi bilioni 1.1.
Kitaifa, Naibu Rais alisisitiza kuwa serikali kuu inazidi kutekeleza miradi inayomzingatia mkulima inayohusisha sera rafiki kama mbolea ya bei nafuu iliyopunguzwa kutoka shilingi 7,500 hadi 2,000, kupunguzwa kwa bei za mbegu kwa nusu, na kuboresha mapato ya maziwa, kahawa na majani chai.