Rais Ruto ataja kampeni za upinzani kuwa siasa potovu

Rais alidokeza kuwa yuko tayari kuwajibikia utendakazi wake wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto aweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa gereza la Kitale, kaunti ya Trans Nzoia.

Rais William Ruto amewapuuzilia mbali viongozi wa upinzani, akiwalaumu kwa kuendeleza kampeni zenye siasa potovu.

Akizungumza leo Ijumaa kwenye siku yake ya tano ya ziara ya maendeleo katika kaunti za Pokot Magharibi na Trans Nzoia, kiongozi wa taifa alisema uzingatiaji katiba umekitwa kwenye haki ya kidemokrasia ya wapiga kura, akiwashtumu wapinzani wake kwa kushindwa kuwasilisha mipango yao kwa taifa.

Rais alidokeza kuwa yuko tayari kuwajibikia utendakazi wake wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.

Akiwa kwenye ziara hiyo aliweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa gereza la Kitale, litakalogharimu shilingi bilioni 4.05,  na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika eneo bunge la Saboti, kaunti ya Trans Nzoia.

Katika shule ya upili ya wasichana ya St Joseph’s, kiongozi wa taifa alisema serikali itajenga ukumbi mpya wa mankuli, madarasa 20 na mabara manne.

“Lengo letu ni kuweka vifaa vya kisasa shuleni ili kufanikish viwango bora vya elimu na kubuni mazingira bora ya masomo kwa wanafunzi wetu,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto yuko kwenye ziara ya siku 10 katika kaunti za Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi.

Share This Article