Waziri wa Fedha John Mbadi ametangaza kuwa atagombea wadhifa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2032.
Amesema yeye anafahamu sana maono na sera za Rais Ruto baada ya kufanya kazi naye kwa karibu tangu alipojiunga na serikali jumuishi na hivyo atastahili kupokezwa kijiti cha urais baada ya Ruto kuondoka madarakani.
“2032, mimi nasimama kama Rais wa Kenya. Na hapo hakuna kubahatisha. Mimi nikiamua kuchukua kitu nitachukua,” alisema Mbadi wakati akizungumza huko Suba Kusini, kaunti ya Homa Bay.
“Ninajua kura inapigwa, inafika mahali, wewe mwenyewe unajijaza. So nitajaza zile zitabaki. Lazima nikuwe Rais wa Kenya wa 6 baada ya President Ruto juu mimi ndiye ninajua Ruto anapeleka Kenya wapi.”
Rais Ruto kwa sasa ameimarisha jitihada za kuwinda muhula wa pili wa kuongoza nchi wakati uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukikaribia.
Ameelezea imani kwamba atashinda uchaguzi huo asubuhi na mapema kwani upinzani, kulingana na yeye, hauna hata chembe ya mpango kando na kaulimbiu za one term.
Kwa upande wao, viongozi wa upinzani akiwemo Rigathi Gachagua wa DCP, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Edwin Sifuna wa vuguvugu la Linda Mwananchi, Dkt. Fred Matiang’i wa Jubilee na Martha Karua wa PLP, miongoni mwa wengine, wameapa kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja kukabiliana na Ruto 2027.