Majengo ya mahakama katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, na maeneo mengine yamefungwa huku muda wa mwisho wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa urais ukikaribia.
Polisi wanashirika doria huku baadhi ya mahakama zikizingirwa kwa utepe ili kuzuia watu kuingia.
Mgombea wa upinzani Brian Mundubile amesema atapinga matokeo ya uchaguzi huo, akitaja kasoro mbalimbali, baada ya kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 38 ya kura.
Rais aliyeko madarakani, Hakainde Hichilema, alishinda muhula wa pili kwa kupata asilimia 60 ya kura.
Mundubile anajificha kutokana na madai ya vitisho dhidi yake, katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi kilichogubikwa na utata, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa kiongozi wa upinzani na kukamatwa kwa watu wengine.
Leo Jumatatu ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais.
Pingizi hilo linaweza kuathiri sherehe za kuapishwa kwa Hichilema, ambazo zimepangwa kufanyika tarehe 1 Septemba.
Siku ya Jumatatu, mawakili waliofika mahakamani waliambiwa waondoke.
Wakili mmoja aliambia BBC kuwa watu watatu wenye silaha walimfuata kwenye gari lake, wakajitambulisha, na kumwagiza aondoke eneo hilo.
Mahakama zilizofungwa ni pamoja na Mahakama Kuu jijini Lusaka, Mahakama ya Juu (ambayo pia ina Mahakama ya Katiba), na mahakama kadhaa za ngazi ya chini.
Taarifa ya BBC