Maafisa wa Polisi wamewakamata washukiwa watano kuhusiana na ghasia zilizoibuka wakati wa kumbukumbu ya mwaka wa kwanza tangu kufariki kwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.
Katika sherehe hizo, sehemu ya kundi moja la watu waliokusanyika katika eneo hilo, ilizua vurugu na kuwasababisha maafisa wa polisi kuingilia kati na kutuliza hali.
“Watano hao Daniel Odhiambo, Gabriel Aloo, Felix Ochieng, Jerry Okello na Edwin Matongo, walitiwa nguvuni kuhusiana na vurugu hizo,” ilisema Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI.
Maafisa wa polisi walipata shoka, visu, na upanga miongoni mwa silaha zingine kutoka kwa washukiwa hao.
Washukiwa hao wanazuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani, huku silaha hizo zikihifadhiwa na zitatumika kama ushahidi kwenye kesi inayowakabili.
DCI imesema inashirikiana na asasi zingine za usalama kuhakikisha usalama kwenye mikutano ya umma.