Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Shauri Moyo, wamemkamata mshukiwa wa ujambazi, anayehusishwa na visa vya wizi katika kaunti ya Nairobi.
Kulingana na polisi, mshukiwa huyo alifumaniwa akimpora mtu simu na shilingi 3,000 pesa taslimu.
Baada ya polisi kumpekua mshukiwa huyo, walipata bastola moja, simu ya rununu na vipande 152 za bangi.
Kupitia ukurasa wa X, Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema mshukiwa huyo anazuiliwa kwenye korokoro za polisi akisubiri kufikishwa mahakamani, huku bastola na bangi zikihifadhiwa kama ushahidi.
Huduma hiyo ya polisi ilielezea kujitolea kwake kukabiliana na wahalifu kote nchini, huku ikitoa wito kwa wananchi kushirikiana na maafisa wa usalama kuhakikisha usalama kwa wote.