Oburu ahimiza nidhamu kwenye usimamizi wa fedha za umma

Oginga alisema kuwa Kenya ina uwezo wa kufikia kiwango cha maendeleo kama kile cha Singapore ila ni sharti ishughulikie changamoto zinazotatiza ukuaji wa kiuchumi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Dkt. Oburu Oginga - Kinara wa ODM

​Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ametoa wito wa kudumishwa kwa nidhamu kwenye usimamizi wa fedha za umma, ili taifa hili lipige hatua zaidi katika kutimiza malengo yake.

Oginga alidokeza kuwa Kenya inapaswa kuhakikisha fedha za umma zinasimamiwa kwa uwajibikaji wa hali ya juu, maadili na nidhamu, ili uchumi wake uimarike na kufikia viwango vya mataifa yaliyostawi kama vile Singapore.

Akizungumza wakati wa mjadala unaoendelea wa kitaifa, Oginga alisema kuwa Kenya ina uwezo wa kufikia kiwango cha maendeleo kama kile cha Singapore ila ni sharti ishughulikie changamoto zinazotatiza ukuaji wa kiuchumi.

Oburu alitoa wito kwa serikali kubuni mazingira mwafaka kwa sekta ya kibinafsi kuendeleza ustawi wa kiuchumi huku ikiunga mkono vyuo vikuu kutekeleza utafiti kuambatana na mahitaji ya sekta hiyo.

“Taifa hili linapaswa kuwawezesha wakulima, vijana, wabunifu na kuimarisha uzalishaji bidhaa na teknolojia,” alisema Oginga.

Alisema ruwaza ya 2060 sio kuhusu kiongozi mmoja, chama chochote cha kisiasa, lakini ni kuhusu Kenya, watoto na wajukuu wake.

Kulingana na Oginga, Kenya inahitaji ruwaza ya kitaifa ya kudumu kuongoza serikali zinazoongoza na kudumisha maendeleo hadi mwaka 2060.

Share This Article