Baraza la Wazee wa Jamii ya Borana, limekanusha madai kwamba limeidhinisha kuunga mkono chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), kinachoongozwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.
Kulingana na Baraza hilo, mwanachama wao aliyekutana na uongozi wa chama cha DCP, hakuwa na idhini ya baraza hilo.
Kwenye mkutano na wanahabari katika kaunti ya Isiolo, uongozi wa baraza hilo ulijitenga na mshauri wake wa kiufundi Yusuf Huka Jillo, ambaye hivi majuzi alishiriki mazungumzo na Katibu Mkuu wa DCP Seneta John Methu nyumbani kwake katika kaunti ya Nyandarua.
Wakati wa mkutano huo, Jillo anadaiwa kuwasilisha mbuzi wanne kama zawadi akisema ametumwa na Baraza la wazee wa jamii ya Borana kuanzisha ushirikiano wa kisiasa na chama hicho.
Kulingana na baraza hilo, Jillo hakuwakilisha wazee hao wala hakuwa na idhini ya kuzungumza kwa niaba yao kuhusu maswala ya kisiasa.
Wakiongozwa na mwenyekiti Mohamed Konso Halo, Naibu Katibu Mkuu Hussein Boru na Mweka Hazima Hassan Shano, wazee hao walipinga madai kwamba wameazimia kujiunga na chama cha DCP.
“Baraza la Wazee wa jamii ya Borana halijatoa maamuzi yoyote ya kujiunga na chama cha Democracy for Citizens Party au chama kingine cha kisiasa. Yusuf Jillo hakutumwa na baraza hili kwenye mkutano na Seneta Methu au kiongozi mwingine wa kisiasa,” alisema Halo katika mkutano huo na wanahabari.
Baraza hilo lilishikilia kuwa halijaunga mkono chama chochote cha kisiasa huku taifa hili likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.