Wazazi washauriwa kuwalinda watoto wao dhidi ya uhuni wa kisiasa

Katibu katika wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema wazazi wanapaswa kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao, elimu na wanaojihusisha nao badala ya kuwaachia walimu jukumu hilo.

Tom Mathinji
2 Min Read
Dr. Raymond Omollo - Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa.

Wazazi wameshauriwa kuwajibika na kuwalinda watoto wao dhidi wanasiasa na makundi ya wahalifu, yanayowalenga kuwatumia vijana kuzua vurugu na shughuli zingine za uvunjaji wa sheria.

Katibu katika wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema wazazi wanapaswa kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao, elimu na wanaojihusisha nao badala ya kuwaachia walimu jukumu hilo.

“Nawasihi wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu ili kushughulikia visa vya utovu wa nidhamu. Vijana wetu hawapaswi kuruhusiwa kuwa maajenti wa ghasia na uhuni wa kisiasa,” alisema Omollo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wazazi wa shule ya upili ya wavulana ya Ober kaunti ya Homa Bay, katibu huyo alionya kuwa vijana ndio huathirika pakubwa wanapohadaiwa kujiunga na ghasia za kisiasa, akiwahimiza wazazi, walimu na viongozi wa jamii kuwaongoza vijana kukumbatia elimu, ujuzi na shughuli za kiuchumi.

Dkt. Omollo alidokeza kuwa misururu ya ghasia ambayo imeshuhudiwa katika shule mbalimbali, ilihitaji ushirikiano dhabiti kati ya wazazi, walimu, wanafunzi na usimamizi wa shule, akiwapongeza wanafunzi wa Ober Boys kwa kudumisha nidhamu akiwataka kuweka malengo yao kwa masomo.

Alisema serikali imejitolea kuimarisha sekta ya elimu kupitia kuongeza ufadhili, kuwaajiri walimu zaidi na kupamua miundombinu ya shule.

Aidha, alidokeza kuwa walimu 100,000 wameajiriwa katika muda wa miaka  mitatu iliyopita, huku walimu 20,000 wakitarajiwa kuajiriwa mwaka huu wa kifedha.

Share This Article